Friday, June 14, 2013

Hii ndo historia ya langa kileo

Langa (wa kwanza, kulia mwa skrini
yako, aliyesimama), aliandika hivi,
"Mkutano wa kuunda baraza la
viongozi wa dini wa kupambana na
madawa. We did it Again, Bringing
more people into Recovery." Januari
2012
Je, unamkumbuka Langa Kileo? Bila
shaka hili ni jina maarufu, hasa kwa
wadau wa masuala ya burudani wa
ndani na nje ya nchi.
Huyu ni mmoja wa matunda ya
shindano la muziki la Coca-Cola Pop
Stars mwaka 2004 ambalo washindi
wake waliounda kundi la Wakilisha.
Mbali ya Langa, wengine ni Sarah
Kaisi ‘Shaa’ na Witness Mwaijaga
`Witness’. Huo ndio uliokuwa
mwanzo wa kung’ara kisanii kwa
wakali hao, ingawa kwa sasa kundi
hilo limesambaratika, kila mmoja
akitamba kivyake.
Lakini kwa bahati mbaya, mmoja
wao, Langa kwa miaka ya hivi
karibuni hakusikika kabisa, jambo
lililomlazimu mwandishi wa makala
haya kumtafuta sababu za ukimya
wake.
Haikuwa kazi rahisi, lakini hatimaye
Langa alipatikana na bila kutafuna
maneno alisema kwamba, alishindwa
kufanya kazi baada ya kuwa `teja’
aliyekubuhu.
Yaani alizama katika matumizi ya
dawa za kulevya kiasi cha kupoteza
kabisa mwelekeo si wa kisanii pekee,
bali hata kimaisha.
“Siyo siri, kilichokuwa kimenifikisha
katika hali hiyo ni dawa za kulevya.
Kwa miaka mitano nilitumia sana
Cocaine, Heroin, bangi na pombe.
Namshukuru Mungu sasa nimerejea
katika hali yangu…
“Siamini kama nimenusurika kwa
sababu madawa yalinitesa, nikafanya
mengi ya ajabu yaliyoichukiza familia
yangu na marafiki ikiwa pamoja na
kuwa mwizi na mkabaji mitaani na
nyakati za usiku,” anasema Langa
ambaye kundi lao la Wakilisha
lilitamba na nyimbo kama
`Unaniacha Hoi’ na `Kiswanglish’.
Anaeleza kwamba, kwake hayo ndiyo
aliyoyaona maisha yanayomfaa,
akidai awali alikuwa amechoshwa
kuishi kwa masharti kutoka kwa
wazazi wake waliokuwa wanampa
mwongozo wa maisha, lakini bila
kujua akadhani `anachungwa’.
Kwamba, umaarufu na ngekewa ya
kuzishika pesa katika umri mdogo
kupitia muziki vilimtia kiburi zaidi,
na hivyo kuamua kujitenga kabisa na
familia yake iliyomlea kwa mapenzi
mazito.
“Niliamini naweza kujitegemea
kupitia kazi yangu ya muziki,
nikajichanganya mtaani,” anasema
kijana huyo aliyetoa kibao chake cha
kwanza, Matawi ya Juu mara baada
ya kusambaratika kwa kundi la
Wakilisha kutokana na kila mmoja
kuamua kujitegemea kimuziki. Na
kweli, Matawi ya Juu ilidhihirisha
kuwa Langa ni moto wa kuotea mbali
katika fani. Aliweza kusimama kwa
miguu yake na kutikisa.
Mwenyewe anasema: “Jina hilo la
Matawi ya Juu lilidhihirisha hivyo
pale video ya kibao hicho ilipotajwa
kuwania Tuzo za MTV Base kwa
upande wa hapa Bongo miaka
michache iliyopita, kisha kutwaa
Tuzo ya Kisima nchini Kenya. “Moto
huo uliwafanya baadhi ya wasanii
wakongwe katika gemu ya Bongo
Fleva kunitafuta na kunipa
majukumu ya kushiriki katika kazi
zao, ikiwemo Chagua Moja ya Farid
Kubanda `Fid Q’.
“Baada ya kuona wakongwe
wamekubali vitu vyangu na kuanza
kunishirikisha…nikapata pia safari za
nje ya nchi. Huko Nairobi (Kenya)
niliweza kufanya kazi na vichwa
vikali vinavyounda Kundi la
Necessary Noise, Naaziz na Wyre
(Kevin Wyre)….”
Anasema mafanikio hayo yalimtuma
kufyatua albamu yake ya kwanza
aliyoipa jina la Langa, akiamini
itampaisha zaidi kimaisha na
kimuziki. Hata hivyo, mambo
yalikwenda kinyume. Anasema
alipoipeleka sokoni, wauzaji
wakubwa waliigomea, hivyo kumpa
wakati mgumu wa kuwaza na
hatimaye kujikuta akiongeza kasi ya
matumizi ya dawa za kulevya.
Siyo siri, kugoma kwa albamu yangu
sokoni kulichangia kasi ya kutumia
dawa za kulevya…niliona ni njia
pekee ya kuondoa mawazo kwa
sababu kazi iligoma, na home
(nyumbani) nilishaharibu.
Sikufanya tena kazi kwa umakini na
kila kazi niliyoitia haikufanya
vizuri….” Anasema kwamba, baada
ya mambo kumwendea mrama, ndipo
alipoanza kuiba vitu nyumbani kwao
kwa lengo la kuviuza na inapotokea
amekosa, alidiriki hata kupiga debe
katika vituo vya mabasi ili mradi
apate fedha za kununua `unga’.
Haikuishia hapo, kwani anasema
alijiingiza katika kundi la wahuni
waliojihusisha na wizi na ujambazi.
“Kwa ujumla nilipoteza mwelekeo.
Maisha yangu yakawa ya kutembea
na kisu kama kitendea kazi changu
katika wizi,” anasema huku akitikisa
kichwa kama ishara ya kujutia
matendo aliyoyafanya kwa msukumo
wa madawa ya kulevya. Anakumbuka
akiwa mtumwa wa `unga’, aliingia
katika mikasa kadhaa ikiwa pamoja
na kupigana na polisi baada ya
kunaswa na dawa hizo haramu.
Katika wizi, chochote alichokikuta
mbele yake kilikuwa halali. Anasema
alikwapua vitu magengeni, madukani
na hata magari yaliyoegesha vibaya
alinyofoa vioo na mashine
zinazosaidia kupandisha na
kushusha vioo ndani ya gari.
“Ni matukio ya aibu.
Yanasikitisha…,” anasema Langa
anayedokeza kwamba, akiwa
mtumiaji wa `unga’, alikuwa
anakutana na wasanii na watu
wengine mashuhuri. Hata hivyo
anakataa kuwataja, akidai ni siri
yake. `Ufufuo’ wa Langa kutoka
katika lindi la mateso ya dawa za
kulevya ulipatikana kuanzia Machi
mwaka huu, baada ya familia yake
kumpeleka kijana wao kwa tiba
maalumu ya kuachana na matumizi
ya `madudu’ hayo. Na kweli, elimu
imemwingia na kujikuta akirejea
ufahamu wake wa kawaida.
Ametangaza kuachana na `unga’,
pombe, sigara na badala yake
amejikita zaidi katika mazoezi ya
kurudisha mwili wake katika hali ya
kawaida. Aidha, amekata shauri la
kuirudia fani yake na tayari ana vitu
vipya, Bombokiata na Mteja
Aliyepata Nafuu.
Anasisitiza kwamba, kutokana na
mateso aliyoyapata, anakusudia
katika siku za baadaye afungue kituo
chake cha tiba ya dawa za kulevya ili
aweze kuwaokoa vijana wengine
wanaoangamia kutokana na
matumizi ya dawa hizo haramu
zinazopigwa vita karibu kote
duniani. “Nimenusurika,
namshukuru Mungu.
Nami najipanga kutaka kuwasaidia
wengine waachane na mateso ya
dawa za kulevya. Pia nichukue fursa
hii kuwaomba msamaha wote
niliowakosea kwa namna moja ama
nyingine wakati nikiwa `teja’,”
anasema Langa, kijana mwenye umri
wa miaka 25.
Je, historia ya maisha ya Langa
ikoje? Anasema Desemba mwaka
1985 jijini Dar es Salaam akiwa
tunda la wanandoa Vanessa Kimei na
mumewe Mengisen Kileo. Alisoma
Shule ya Msingi Olympio na
Sekondari ya Loyola, zote za jijini
Dar es Salaam.
Hata hivyo, akiwa kidato cha pili
alihamishiwa Kampala, Uganda
katika Shule ya Vienna na baadaye
Shule ya Hillside International
Academy, huko huko Uganda.
Baadaye alirejea nchini na kujiunga
na masomo ya Stashahada ya Masoko
katika Chuo cha Biashara Dar es
Salaam (CBE), Kampasi ya Dodoma

No comments:

Post a Comment