Tuesday, May 7, 2013

Aliyerusha bom apatikana


DEREVA wa pikipiki maarufu kama
bodaboda, Victor
Ambrose,anatuhumiwa kurusha
bomu katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia
ya Olasiti jijini Arusha,
lililosababisha vifo vya watu wawili
na wengine karibu 70 kujeruhiwa.
Ambrose mwenye umri wa miaka 20
na mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha,
anashikiliwa pamoja na watuhumiwa
wengine tisa, wakiwemo raia wanne
wa Saudi Arabia kwa mahojiano zaidi
ya kuhusika na tukio hilo.
Taarifa zilizopatikana jana jioni,
zilieleza kuwa raia hao wa Saudi
Arabia, waliingia nchini Jumamosi
usiku kwa ndege kupitia Uwanja wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na
baada ya tukio Jumapili, waliondoka
nchini kupitia mpaka wa Tanzania
na Kenya, Namanga.
Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi, ilitoa taarifa hiyo jana
bungeni na kueleza namna uhalifu
huo ulivyotendeka kanisani hapo
juzi, muda mfupi baada ya ibada
kuanza.
Kwa mujibu wa Waziri Nchimbi,
uchunguzi wa awali unaonesha kuwa
mlipuko huo ni bomu. Hata hivyo
uchunguzi wa kubaini aina ya bomu
lililotumika, unaendelea kufanywa na
Polisi na wataalamu wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ).
“Hadi sasa watuhumiwa sita
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Miongoni mwao ni Victor Ambrose
mwenye umri wa miaka 20 dereva wa
bodaboda…ambaye anatuhumiwa
kurusha bomu hilo. “Watuhumiwa
wengine watano waliokamatwa ni
raia wa kigeni na Mtanzania mmoja
ambao wanashikiliwa kwa
mahojiano,” alisema Dk Nchimbi.
Waziri alitaja waliokufa katika tukio
hilo kuwa ni mtoto mwenye umri wa
miaka 16, James Gabriel, aliyefariki
usiku wa jana na Regina Kurusei
(45), mkazi wa Olasiti aliyefariki siku
ya tukio wakati akipatiwa matibabu
katika Hospitali ya Mount Meru.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Magesa Mulongo, alisema
waliokamatwa wamefikia 10, na raia
hao wa nje ni wa Saudi Arabia.
Alisema pia mtu wa tatu alifariki
lakini hakumtaja jina. Kaimu Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru,
Dk Mariam Murktadha, alifafanua
kuwa kijana Gabriel, alifia Uwanja wa
Ndege wa Arusha, akiwa njiani
kupelekwa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Aliongeza kuwa majeruhi walikuwa
66 na hivi sasa wamebaki 34 na
wengine wameruhusiwa.
Kwa mujibu wa Dk Nchimbi,
majeruhi walikimbizwa Hospitali ya
Mount Meru, wengine Hospitali ya St
Elizabeth kwa Father Babu, Hospitali
ya Selian na mwingine alipelekwa
katika Hospitali ya Dk Wanjara,
Mianzini.
Bomu lilivyorushwa
Akielezea tukio hilo, Waziri Nchimbi
alisema lilirushwa wakati mgeni
rasmi, Balozi wa Vatican nchini na
Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu
Fransisco Padilla, akiwa ametoka nje
ya kanisa akijiandaa kukata utepe
kama ishara ya uzinduzi.
Alisema mtu huyo alirusha kitu
chenye ukubwa wa ngumi, kwenda
eneo kulipokuwa na mkusanyiko wa
watu na baada ya kutua, kulitokea
kishindo na mlipuko mkubwa.
Inakadiriwa uzinduzi huo wa Kanisa,
ulihudhuriwa na watu zaidi ya 2,000.
Alisema viongozi wa dini na Serikali
waliohudhuria ibada hiyo,
hawakupata madhara yoyote
kutokana mlipuko huo. Udini
Amewasihi Watanzania kuwa
watulivu wakati vyombo vya dola
vikiwasaka walihusika na shambulio
hilo.
Aidha ametaka kila mwenye taarifa
za kuwezesha kukamatwa wahalifu
hao azitoe Polisi. Kwa mujibu wa
Waziri Nchimbi, siku za hivi karibuni
kumekuwepo jitihada kubwa za watu
wachache wasioitakia mema nchi,
kutaka kupandikiza chuki za kidini
miongoni mwa Watanzania na kuleta
mapigano na mauaji.
“Sina shaka kuwa shambulio la
Arusha ni sehemu ya mikakati hiyo
miovu,” alisema bungeni na
kusisitiza kwamba Serikali itachukua
hatua kali kwa mtu yeyote bila kujali
hadhi na nafasi yake katika jamii.
Wanasiasa waonywa
Wakati huo huo, Waziri Nchimbi
amekemea wanasiasa wanaotafuta
umaarufu wa kisiasa kupitia tukio
hilo, akisisitiza kwamba Serikali
isilaumiwe kwa hatua kali za kisheria
itakazochukua dhidi ya viongozi wa
aina hiyo.
“Kokote duniani tukio la kushitukiza
linalosikitisha na kuhuzunisha kama
hili linapotokea, wananchi wote
huungana na kuwa wamoja kama
taifa na kulaani wahusika na
kuwafariji waathirika wa tukio hilo,”
alisema Dk Nchimbi.
Akikemea wanasiasa wanaotumia
matukio kujinufaisha, huku akitoa
mfano wa Marekani na kusema
mgombea mmoja wa urais wakati wa
uchaguzi mkuu wa mwaka 2012,
aliishutumu Serikali kutokana na
kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani
nchini Libya.
“Ni wazi kuwa mgombea huyo
alichukua tatizo lile kama ajenda ya
kisiasa. Hata hivyo alishutumiwa
vikali na Wamarekani wenzake kwa
kuelezwa kuwa ni mtu mwenye
kukosa kabisa misingi ya uaminifu na
uzalendo kwa taifa lake.”
“Serikali inasikitishwa sana na
wanasiasa wa aina hii, ambao
wanajitokeza nchini na kutafuta
umaarufu wa kisiasa kwa gharama za
maisha ya Watanzania…Serikali
isilaumiwe kwa hatua kali za kisheria
itakazochukua dhidi ya viongozi wa
aina hii, ambao maslahi yao ni
muhimu kuliko maisha ya
Watanzania,” alisema.
Dk Nchimbi alilaani waliohusika
kufanya uhalifu huo na kusema
Serikali kwa nguvu zote itahakikisha
watuhumiwa wote waliohusika na
kushiriki kwa namna yoyote katika
tukio hilo, wanasakwa popote walipo
na kufikishwa katika vyombo vya
sheria.
“Tunawataka viongozi wa kisiasa,
kidini na wananchi wote kwa ujumla
kila mmoja kwa nafasi yake
kuwajibika, ili kuhakikisha kuwa nchi
yetu inaendelea kuwa kisiwa cha
amani na utulivu,” alisema.

No comments:

Post a Comment